Na Mwandisi wetu DAR ES SALAAM
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe, amewataka watendaji katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuwekeza zaidi katika suala la Afya kinga sambamba na kutilia mkazo wa ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya katolea huduma.
Dkt. Magembe ametoa maelekezo hayo muda mfupi, mara baada yakufanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni na kukagua shughuli za kiutendaji kwenye Hospitali hiyo kisha kufanya mkutano wa pamoja ulio wakutanisha watendaji wa Mkoa na kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nataka mhahakikishe mnafuatilia utoaji wa huduma za kinga na tiba kwenye maeneo yenu, lakini sula lingine ni usimamiaji wa karibu wa mapato na matumizi ya vituo vya tiba pamoja na vyanzo vingine vyote vya mapato” Amesema Magembe.
Dkt. Magembe amesema, Mkoa wa Dar es Salaam, ni lazima asilimia 60 ya mapato ya ndani yaelekezwe kwenye miradi ya maendeleo inayoonekana kwa macho na yenye matokeo chanya katika kutatua changamoto za wananchi.
Kuhusiana na utatuzi wa kero kwa wananchi Dkt. Magembe amewaagiza watendaji hao, kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kupokea kero za wananchi ikiwepo masanduku ya maoni pamoja na namba za simu za viongozi zibandikwe kwenye mbao za matangazo maeneo ya kutolea huduma sehemu za wazi.
Naibu katibu mkuu ametumia nafasi hiyo kuwaagiza wakurugenzi wote kufanya ukaguzi kwenye vituo vya tiba, na maeneo yote yanayokusanya fedha za serikali na kuangalia kama kuna matumizi ya fedha yamefanyika kabla ya fedha hizo kuwasilishwa benki, aidha watakao bainika kufanya hivyo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Naibu Katibu Mkuu huyo ambaye yupo katika ziara ya kikazi kwenye Mkoa huo, amewaagiza waganga wakuu wa Mikoa kote nchini, kuhakikisha wanawasilisha taarifa za vizazi na vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwenye vikao vya menejimenti vya Sekreatriati za mikoa na waganga wakuu wa halmashauri kufanya hivyo kwenye vikao vya menejimenti ndani ya halmashauri ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kuchukua hatua za haraka za kiutendaji.
Katika ziara hiyo, ambayo ilikwenda sambamba na mafunzo kwa Wakurugenzi yaliyo endeshwa na Dkt. Grace, Watendaji hao wamempongeza kwa hatua hiyo, kwani imewasaidia kujua mambo mengi hasa katika utaratibu wa utoaji wa huduma za afya, na katika kuhitimisha Naibu Katibu Mkuu amemuelekeza Mfamasia katika Halmashauri ya Kigamboni kuendeleza elimu hiyo.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Naibu Katibu Mkuu, toka ateuliwe kushika wadhifa huo mapema mwaka huu, akichukua nafasi iliyo achwa wazi na Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Afya.
MWISHO
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.