Na Fred Kibano – OR TAMISEMI
Mkurugenzi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema Mpango kazi wa kuboresha huduma za afya ya msingi utasaidia kutoa huduma bora za afya katika ngazi ya msingi nchini kote.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kuhitimisha kikao kazi cha kuandaa Mpango huo wa afya ulioandaliwa kwa pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya na Wadau wengine hivi leo tarehe 4.11.2022 Jijini Dodoma
Amesema Mpango huo utawasaidia Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Kamati za Afya za Mikoa na Wilaya kuweza kusimamia utekelezaji wa utoaji wa huduma kwenye vituo mbalimbali vya afya nchini.
Aidha, Dkt. Kapologwe amesema Mpango huo pia utakuwa na viashiria ambavyo vitapima ubora wa utoaji wa huduma za afya kwa mujibu wa Mwongozo wa Wizara ya Afya Tanzania.
Ametoa rai kwa watumishi wote nchini kuzingatia kanuni, sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo inalenga katika utoaji wa huduma za afya ili ifikapo mwaka 2030 Tanzania kama nchi iwe imefikia hatua ya afya kwa wote, afya iliyo bora na inayopatikana.
Kwa upande wake Dkt. Revocatus Baltazar Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole Jijini Dodoma amesema Mpango huo wa afya kwao utawasaidia kutoa huduma za afya ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya katika kuboresha miundombinu ya afya na kuwa rafiki kwa wateja, kuongeza ushirikishwaji wa jamii kwa huduma zinazopatikana na jamii inavyoweza kusaidia kuboresha huduma za afya kwenye maeneo yao.
Lakini pia utasaidia uwajibikaji wa watumishi, upatikanaji wa dawa kwa kujua aina ya dawa zinazotakiwa kulingana na mahitaji pamoja na vifaa vya maabara.
Naye Raymond Shishira Mratibu wa Programu ya PS3 Plus Tanzania amesema Mpango huu wa miaka mitano (2020 – 2025) utasaidia mifumo kuwasiliana na mifumo mingine lakini pia utasaidia upatikanaji wa taarifa mbalimbali za afya na namna ya kuzitumia hali itakayoifanya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa mtoa huduma mzuri nchini.
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.