Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph Pombe Magufuli ameipongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa usimamizi wenye weledi katika ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za Afya Nchini.
Ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mbonde katika Halmashauri Mji wa Masasi, Mkoani Mtwara kwa niaba ya vituo 352 vya kutolea huduma nchini ambavyo vimejengwa katika Halmashauri zote nchini.
Mhe. Magufuli amesema kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma lakini Wizara hizo mbili zimeweza kusimamia kwa weledi utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo.
“Kutengwa kwa fedha ni sula la msingi lakini usimamizi wa fedha ni suala muhimu sana hivyo nimeridhishwa na usimamizi uliofanywa na Wizara hizi mbili ambapo ujenzi umefanyika kwa kiwango kikubwa na usimamizi huo unaacha alama kwa nchi na kupunguza kero za miundominu ya afya nchini” Amesema Mhe. Magufuli
Mhe. Magufuli amewapongeza watumishi wa OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya kwa kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia na kuhakikisha vituo vya afya vinakamilika kwa wakati na viwango vya juu na kuanza kutoa huduma kwa jamii ili kuwahudumia wananchi maskini nchini.
“Panapostahili kupongezwa napongeza hadharani bila kificho na sitasubiri mpaka mtu afe, kwa kweli Wizara hizi mbili wamesimamia kazi ya ujenzi wa vituo vya afya kwa umakini mkubwa na wamefanyakazi nzuri” Amesisitiza Mhe. Magufuli
Amesema kuwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 wameweza kujenga Wodi ya Wazazi, Jengo la Maabara, Chumba cha kuifadhia maiti, chumba cha Mionzi na Jengo la upasuaji hivyo nimeridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo katika Sekta ya afya
Mhe. Magufuli amewapongeza Wataalam wa afya nchini kwa kufanyakazi kwa weledi na moyo wa kujitolea na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii maskini ambao ndio wenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya nchini.
Aidha Mhe. Magufuli amefafanua kuwa gharama zilizotumika katika ujenzi wa vituo 352 ni shilingi bilioni 184 hivyo amewashukuru wananchi, wadau wa maendeleo kwa kujitoa kwa moyo kuleta maendeleo katika Sekta ya afya nchini.
Wakati Huohuo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa sekta ya afya ni eneo linalogusa wananchi wa hali ya nchini hivyo serikali iliamua kuwekeza katika sekta ya afya ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Amesema tangu uhuru kulikuwa na Hospitali za Serikali 77 katika Halmashauri 185, vituo vya afya 535 ambapo viliyokuwa na uwezo wa kufanya upasuaji ni vituo vya afya 118 hali hii ilikuwa ikisababisha vifo vya mama na mtoto pale anapohitaji kujifungua kwa njia ya upasiaji kwa kuwa walikuwa wakitembea muda mrefu kufuata huduma hizo katika Hospitali za Rufaa.
Aidha Mhe Jafo amesema katika miezi 18 ya ujenzi wa vituo vya afya nchini Serikali imeweza kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya ambapo mpaka sasa vituo 352 vimeweza kujengwa na vinaweza kufanya huduma ya upasuaji.
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.