Sekta zote nchini zatakiwa kushiriki katika kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa ili kuisaidia jamii katika kujiepusha na madhara makubwa yanayojitokeza na kupunguza gharama kubwa zinazotumika kwa matibabu.
Hayo yamesemwa na wadau wa afya wanaojishughulisha na magonjwa yasiyoambukizwa kwenye Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa mwaka 2015/2020 wa udhibiti wa magonjwa yasiyoambukizwa na kutoa mwelekeo wa nini kifanyike kwa sasa na baadaye kiichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa , Jijini Dodoma
Wakichangia mada ya nini kifanyike kupunguza magonjwa yasiyoambukizwa wadau hao wamesema Serikali inajukumu ya kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa kwa kujenga miundombinu ya msingi, kufanya utambuzi wa haraka wa magonjwa na kutoa tiba kwa wakati kwa jamii ili kudhibiti magonjwa hao.
Akifafanua zaidi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. James Kiolowe amesema kuna haja ya kushirikisha Sekta mbalimbali katika kupunguza changamoto mbalimbali zinazosababisha magonjwa yasiyoambukizwa nchini ili kila mmoja awe na jukumu la kulinda afya za jamii nchini.
“Umefika wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuwa wao ni watunga sera washirikishe Wizara nyingine kama Kilimo, ardhi, Mazingira ili kuhakikisha wanahusika katika kutatua changamoto za afua za afya na kupunguza magonjwa yasiyoambukizwa nchini “Anasema Kiolowe
Wakati Huohuo Dkt. Msafiri Kabulwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ameitaka jamii kushirikishwa kwa kina juu ya madhara yatokanayo na magonjwa yasiyoambukizwa nchini ili kupunguza vifo vya vijana na watoto ambao wengi wamekuwa wakiadhirika na magonjwa hayo.
“Ufike wakati jamii ishirikishwe kikamilifu katika kuhakikisha wanadhibiti magonjwa ili kupunguza vifo kwa jamii. kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba ” Anafafanua Kabulwa
Naye Katibu wa Chama cha Kisukari Tanzania Prof.Kaushik Ramaiya amesema kuwa upo umuhimu wa jamii kupatiwa elimu juu ya madhara yatokanayo na magonjwa yasiyoambukizwa, hii itasaidia kupunguza vifo na gharama ya matibabu kwa jamii.
“Wananchi wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika kutafuta matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza wakati elimu ndio msingi wa kuwasaidia kujikinga na Maradhi mfano jamii inatumia gharama kubwa sana kumtibu mgonjwa mwenye kisukari kuliko kuzuia ugonjwa huo.”Anafafanua Profesa Kaushik
Aidha Rais wa Chama cha madaktari wa meno Tanzania Dkt. Ambige Mwakatobe amesema kunaumuhimu wa jamii kuhakikisha wanafuata ulaji wa vyakula vinavyofaa ili kupunguza magonjwa yasiyoambukizwa kama vile kisukari na kansa.
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.