Na Atley Kuni- MANYARA.
Serikali imepongeza juhudi za usafi wa mazingira katika shule za mkoa wa Manyara chini ya usimamizi wa uongozi wa Mkoa huo kwenye kutekeleza ajenda ya usafi mazingira katika Shule na kwenye Jamii.
Juhudi hizo zimeshuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia afya, Daktari Dorothy Gwajima alipofanya ziara katika Mkoa huo akiwa na wataalam wa Ofisi hiyo kwa lengo la kujionea hali ya utekelezaji wa elimu ya afya na mazingira katika shule zinazomilikiwa na Serikali pamoja na taasisi Binafsi.
Akiwa katika shule ya kutwa ya Babati Sekondari, aliusifu uongozi wa Shule kwa kuzingatia kanuni za afya mashuleni kwa jinsi walivyoweza kuwapanga kwa nafasi wanafunzi katika Mabweni wakiwa wameacha nafasi ya kutosha kutoka kitanda kimoja na kingine pia usafi wa vyoo ukiwa wa viwango na pia wakiwa wamezingatia uwekaji wa vyombo vya maji tiririka na sabuni kila eneo la shule.
“Nimekagua hatua kwa hatua kuona jinsi gani mnatekeleza miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya suala la Afya Mazingira na kwa kweli sina budi kusema mmenikosha sana na hali usafi, yaani chooni ni kusafi kiasi hata huwezi kusikia harufu yoyote, mimi niwatie moyo, endeleeni na usafi huu”, alisema Dkt. Gwajima.
Akiwa katika Shule hiyo ya Babati Day, yeye pamoja na mtaalamu wa lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, walikula chakula kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya Wanafunzi kwa lengo la kujionea ubora wa chakula kinachotumiwa na wanafunzi hao.
“Wali huu ni mtamu sana, hivi haya maharage mmenunua wapi”, alisikia Naibu Katibu Mkuu, huku akipeleka Kongole kwa mpishi wa shule hiyo kwa kuwajali wanafunzi na kuwataka kujizatiti katika suala la mboga za majani kwa kuhakikisha Uongozi wa Shule unaratibu kulima mboga mboga kwani wana maeneo mazuri yanayoweza kustawisha mboga za majani kwa wingi.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Singe na Hayatul Islamiya, ambazo zote zinamilikiwa na taasisi za dini, Naibu Katibu Mkuu hakusita kuonesha furaha yake kwa namna taasisi hizo zilivyoweza kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali hususan kwenye kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, ambapo aliweza kujionea Miongozo ikiwa imebandikwa katika shule hizo, lakini pia wanafunzi wakiwa wamechukuwa tahadhari zote za kujilinda dhidi ya maradhi ya ugonjwa huo.
Kwa upande wao uongozi wa shule hizo kwa Nyakati tofauti, waliihakikishia Serikali kuendeleza ushirikiano wao wa karibu katika kutekeleza maagizo yote na miongozo inayotolewa na Serikali katika kutekeleza wajibu wao.
“Ndugu Naibu Katibu Mkuu, naomba nikuhakikishie kuwa, sisi kama shule za taasisi za dini, tutaendelea kushirikiana na Serikali bega kwa bega na kufuata maagizo yote yanayotolewa kwa mustakabali mzuri na thabiti wa afya za Wanafunzi wetu na na ufanisi wa Serikali yetu. Alisema Mkuu wa Shule hiyo Padre Joseph Sakilu.
Naye Mkuu wa Shule ya Hayatul Islamiya Hussen Mwinami alisema, kama shule tayari walishawapokea wanafunzi wote wa kidato cha sita watakaoanza mitihani yao mwishoni mwa mwezi Juni, 2020, lakini pia wamesha weka mazingira rafiki na salama kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi watakaoanza masomo yao tarehe 29 Juni, 2020.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Afisa Elimu wa Mkoa huo, Bw. Samson Hango, alimuahidi Naibu Katibu Mkuu kuendelea kushirikiana katika utendaji kazi na wataalam wa Afya na taasisi zote zenye mapenzi mem ana suala la usafi wakati wote ili kuhakikisha mkoa huo unaendelea kuwa kinara kwenye suala la usafi wa mazingira katika nyanja zote huku wakiahidi kufuatilia na kuhakikisha kasoro ndogo ndogo zote zilizobainika wakati wa ziara zinatatuliwa mara moja.
Ujumbe huo kutoka Ofisi ya Rais–TAMISEMI, ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, ulifanya ziara ya kutembelea na kukagua Shule za Sekondari zilizopokea wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajiwa kuanza mitihani yao ya kuhitimu kuanzia Juni, 29, 2020. Katika ziara hiyo Shule na Vituo vya afya vilivyofikiwa na ziara hiyo ni pamoja na Aldergate Sekondari, Babati Day Sekondari na Kituo cha Afya Mutuka, maeneo mengine ni Singe Sekondari, Bonga Sekondari pamoja na Hayatul Islamiya Sekondari.
MWISHO.
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.