Mratibu wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Mtoto RMNCH-UNFPA na Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi. Dinah Atinda amesitisha safari za nje ya kituo, mikutano, semina na likizo kwa muda wa mwezi mmoja kwa wauguzi wa Kituo cha Afya cha Malampaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu.
Ametoa maagizo mara baada yakutembelea kituo hicho na kukuta huduma za afya zikiwemo za akina mama kujifungua zikifanywa na wahudumu wa afya (Medical Attendant) wakati wauguzi wote wakiwa kwenye semina na mikutano mbalimbali jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa majukumu ya kazi.
“Ni hatari sana muhudumu wa afya (Medical Attendant) kuwahudumia wagonjwa akiwa peke yake bila usimamizi wa muuguzi kwa kuwa anaweza kusababisha madhara au kifo kwa mgonjwa na kushindwa kutoa maelezo sahihii juu ya chanzo cha kifo hicho” Amesema Bi. Atinda.
Bi. Atinda amefafanua kuwa jukumu la kuwahudumia wagonjwa katika Zahanati na Vituo vya afya ni la Wauguzi na Madaktari na si kazi ya wahudumu wa afya hivyo wanawafanya kutotimiza majukumu yao ya kufanya usafi wa mazingira na majengo.
Ameendelea kusema Serikali imetumia fedha nyingi katika kutengeneza miundombinu ya afya na vifaa na vifaa tiba hivyo ni muhimu kila mmoja katika nafasi yake akatimiza majukumu ya kazi aliyopangiwa ili kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.
Amesema wauguzi ni kada muhimu na asilimia zaidi ya 80 ya huduma za afya nchini zinatolewa na wauguzi hivyo ni vyema wakafanyakazi kwa weledi na kwakufuata misingi ya taaluma yao ili kutoa bora na kupunguza vifo vinavyoweza kuzulika kwa jamii.
“Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kutokuwepo kazini bila taarifa, kutokupanga utaratibu wa kazi (Roster) unaozingatia miongozo na kuwapanga wahudumu wa afya zamu bila wauguzi wenye ujuzi suala hili halikubaliki” Amesisitiza Bi. Atinda
Amesisitiza inasikitisha Kituo cha afya cha Malampaka kina watumishi 23 lakini waliokutwa kazini ni 7 wwengine wakiwa kwenye ziara, mafunzo, semina na mikutano, hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma za afya kwa jamii.
Wakati huohuo Bi. Atinda amesitisha safari, semina mikutano na likizo kwa muda wa mwezi mmoja kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Maswa na Mratibu wa afya ya uzazi na Mtoto wa Mkoa na Wilaya na kuwataka kusimamia na kutatua changamoto zilizopo katika kituo hicho.
Amezitaka Timu za usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kusimamia ujenzi wa vituo viwili vitakavyojengwa na kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vilivyojengwa katika Mkoa wa Simiyu vinaanza kufanyakazi.
Aidha amewataka waganga wafawidhi wa vituo kuhakikisha wanasimamia usafi, utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi ili vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinaboreka na kuwavutia wananchi kuja kupata huduma hiyo.
Na. Angela Msimbira MASWA
PO-RALG
Postal Address: 1923
Telephone: +255 26 232 1 234
Mobile: +255 735160210
Email: james.tumaini@tamisemi.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.